AHLUL BAYT WALIO PAMOJA NA QUR'AN

Imam Ali bin Abi Talib (a.s.) amezaliwa ndani ya Al' Kaaba siku ya Ijumaa, tarehe kumi na tatu Rajab mwaka wa thalathini (mwaka wa ndovu).

Wamekhitilafiana waandishi wa tarikh kujuwa tarehe aliyopigwa dharba Imam Ali, baadhi ya kauli hizo zasema:

Alipigwa dharba tarehe 17 usiku wa kuamkia Ijumaa mwezi wa Ramadhan, akafishwa usiku wa kuamkia Jumapili tarehe 19 Ramadhan.

Alipigiwa dharba tarehe 19 usiku, akafishwa tarehe 21 Ramadhan mwaka 40.

Alipigwa dharba kuamkia tarehe 21, akafishwa tarehe 23 Ramadhani.

Alipigwa dharba kuamkia tarehe 23, akafishwa tarehe 25 Ramadhan.

Taz: Kashful Ghumma J. 2 Uk. 63

Riwaya nyingine zinasema kuwa:

Alipigwa dharba asubuhi ya tarehe 17 Ramadhan.

Alipigwa dharba asubuhi ya tarehe 19 Ramadhan, mwaka 40 Hijra.

Taz: Suratul Aimmatil Ithna Ashar J. 1 Uk 452

Abdur Rahman bin Muljam alikutana na msichana mmoja katika khawariji aitwaye Qatwam, ambaye baba yake na kaka yake waliuliwa na Imam Ali katika vita vya Nahrwan. Msichana huyo alikuwa mzuri kupita kiasi, Abdur Rahman alipomtaka Qatwam, alimjibu: "Kama utaweza kunipoza moyo wangu utanipata" Akamuuliza: "Ni lipi litakalo kupoza moyo wako?" Akajibu: "Unipe dirham alfu tatu, mtumishi mmoja, mjakazi, mwimbaji, na umuue Ali bin Abi Talib. Abdur Rahman bin Muljam akasema: "Hayo mengine yote ni mepesi sana, lakini hili la kumuua Ali, ni dalili ya kuwa umenikataa. Kwa sababu haiwezekani kumuua Ali nami nikasalimika, tukaweza kuoana".

Ilipofika siku hiyo, kwa kauli zilivyo khitilafiana, kama ulivyoona hapo juu, Abdur Rahman bin Muljam akatimiza lengo lake.

Imam Ali amezikwa Kufa katika nchi ya Iraq.

Taz: Kashful Ghumma J. 2 Uk. 62

Tabaqatul Kubra J. 6 Uk. 12

Tadhkiratul Khawas Uk. 179

Imam Hasan bin Ali (a.s.) amezaliwa katika mji wa Madina, tarehe kumi na tano Ramadhan mwaka wa tatu Hijra'.

Mu'awiya alipotaka kumtawalisha mwanawe Yazid, alitumia mbinu, akamjenga Juuda bint Al'ash'a'th bin Qays. Huyu alikuwa mke wa Imam Hasan (a.s.). Muawiya akampa sumu ili amtilie Imam Hasan. Na endapo atamuua, basi atamfanyia mambo mawili, la kwanza atampa dirham laki moja na la pili atamuoza mwanawe, Yazidi.

Imam Hasan akapewa sumu hiyo na baada ya hapo alibaki siku arobainni akafariki dunia! Amekufa mfungo tano mwaka 50 Hijra.

Taz: Kashful Ghumma J. 2 Uk. 207

Tadhkiratul Khawas Uk. 211

Wengine wanasema: Amekufa mfungo sita mwaka 49 Hijra.

Taz: Tadhkiratul Khawas Uk. 211

Baada ya kufa Imam Hasan Juu'da alipeleka ujumbe kwa Yazidi wa kutaka kuolewa naye kama walivyoahidiana na baba yake Mu'awiya, Yazidi aliruka na kusema: "Hukuweza kumhurumia Hasan utanihurumia mimi!!? Kama umeweza kumuua yeye mimi utanimaliza mara moja, Yazid akakataa kumuoa.

Imam Husein bin Ali (a.s.) amezaliwa katika mji wa Madina tarehe tatu Shaaban mwaka wa nne Hijra. Imam Husein (a.s.) ameuliwa mwezi kumi Muharram siku ya Ijumaa (wengine wanasema Jumamosi) mwaka wa sitini na moja Hijra. Imepokewa kutoka kwa Anas kwamba Mtume (s.a.w.) amesema: "Mwanangu Husein atauliwa katika nchi ya Iraq, yeyote miongoni mwenu atakaekuwapo, basi asimame kumnusuru.

Taz: Dhakhairul Uq'baa Uk. 146.

Imepokewa kwa mama Ummu Salama (mkewe Mtume) anasema: "Nilimuona Mtume (s.a.w.) akikipangusa kichwa cha Imam Husein na huku akilia. Nikamuuliza: "Unalilia nini!" Akasema: "Hivi sasa amenijulisha Malaika Jibril kuwa: Mtoto wangu huyu atauliwa katika ardhi litwayo "KARBALA" kisha akanipa gao la udongo na akaniambia: 'Huu udongo ndipo mahala atakapouliwa, utunze, siku yoyote utakapogeuka kuwa mwekundu basi jua yakwamba amekwisha uliwa".

Taz: Dhakhairul' U'qbaa Uk. 147

Albidayatu J. 3 Uk. 174

Albidayatu Wannihaya J. 6 Uk. 230

Tarikhul Islam J. 3 Uk. 10

Almustadrak J. 3 Uk. 176

Kama ambavyo, siku aliyouliwa Imam Husein mbingu zilimlilia, na alama ya kuonyesha kuwa zinamlilia ni wekundu unao onekana kwenye mawingu. Kwa hiyo, Imam Husein (a.s.) analiliwa na mbingu mpaka leo hii.

Taz: Tafsirul Qurtubi J. 16 Uk. 14

Imam Ali bin Husein (a.s.) amezaliwa katika mji wa Madina tarehe tano Shaaban mwaka thalathini na nane Hijra, kabla ya kufishwa babu yake (Imam Ali) kwa miaka miwili. Imam Ali bin Husein amefariki mwaka wa tisini na nne Hijra, akazikwa katikamji wa Madina katika kiwanja kitakatifu cha Baqii.

Imam Muhammad bin Ali (a.s.) amezaliwa katika mji wa Madina tarehe tatu mfungo tano (wengine wanasema tarehe moja Rajab) mwaka hamsini na saba Hijra, kabla ya kuuliwa babu yake Imam Husein kwa miaka mitatu. Wamekhitilafiana mwaka aliofia kama hivi:

Amefishwa mwaka 114 Hijra.

Amefishwa mwaka 117 Hijra.

Amefishwa mwaka 118 Hijra.

Imam Ja'far bin Muhammad (a.s.) amezaliwa katika mji wa Madina tarehe 16 mfungo sita (wengine wanasema tarehe moja Rajab) mwaka 80 Hijra. Imam amefishwa katika mji wa Madina mwaka 149 Hijra, amezikwa pamoja na baba yake na babu yake katika viwanja vitakatifu vya Baqii.

Taz: Siiratul' Aimmatil Ithna Ashar J. 2 Uk. 225

Imam Musa bin Ja'far (a.s.) amezaliwa katika kijiji cha "AB'WAA" kilicho kati ya Makka na Madina, mahala ambapo kaburi la Mwana Amina bint Wahab mama yake Mtume (s.a.w.) lilipo. Amezaliwa mwaka 128 Hijra (wengine wanasema mwaka 129). Imam Musa amefariki mwaka 188 Hijra baada ya kutiwa jela na Haruna Rashid kwa miaka kumi moja.

Taz: Tadhkiratul Khawas Uk. 350.

Imam Ali bin Musa (a.s.) amezaliwa katika mji wa Madina. Wamekhitilafiana kujuwa tarehe aliyozaliwa kama hivi:

Amezaliwa mfungo pili mwaka 148.

Amezaliwa mfungo tatu mwaka 148.

Amezaliwa mfungo sita mwaka 148.

Amezaliwa mwaka 153.

Kifo cha Imam Ali bin Musa kimetokana na maji ya matunda yenye sumu aliyopewa na Maamun. Baada ya kunywa Imam alibaki siku mbili kisha akafariki dunia, mwaka 203 wengine wanasema mwaka 202 na wengine wanasema mwaka 206.

Taz: Siiratul' Aimmatil' Ithna Ashar J. 2 Uk. 341

Imam Muhammad bin Ali (a.s.) amezaliwa katika mji wa Madina, tarehe kumi na tisa Ramadhan mwaka 195 Hijra. Amefariki Imam Muhammad mwaka 220 wengine wanasema mwaka 225

Taz: Siiratul' Aimmatil' Ithna Ashar J.2 Uk. 448.

Imam Ali bin Muhammad (a.s.) amezaliwa Rajab mwaka 214 Hijra umbali wa maili tatu hivi kutoka katika mji wa Madina. Imam Ali bin Muhammad ameuliwa kwa sumu mwaka 254 Hijra.

Imam Hasan bin Ali (a.s.) amezaliwa katika mji wa Madina mwaka 231 Hijra. Imam Hasan bin Ali amefariki siku ya Ijumaa tarehe nane mfungo sita mwaka 260 na akazikwa mahala alipozikwa Baba yake.

Imam Muhammad bin Hasan (a.s.) amezaliwa tarehe kumi na tano Shaaban mwaka 255 Hijra, wengine wanasema tarehe ishirini na tatu Ramadhan mwaka 258 Hijra. Imam Muhammad bin Hasan yuko hai mpaka sasa, alipofiwa Baba yake alikuwa na umri wa miaka mitano.

Hawa ni Maimam kumi na wawili katika AhIul Bayt (a.s.) walio pamoja na Qur'an. Amesema Mtume (s.a.w.) "Dini itaendelea kuwa imara mpaka isimame kiama, na mtasimamiwa na viongozi kumi na wawili, wote katika Maquraishi".

Taz: Sahihi Muslim J. 6 Uk. 3-4

Sahihi Bukhari J. 4 Uk. 165

Sunan Abi Daud J. 3 Uk. 106

Musnad Ahmad J. 5 Uk. 86-90

Kanzul Ummal J. 13 Uk. 26-27

Hilyatul Awliyaa J. 4 Uk. 333

Na ameonya Mtume (s.a.w.) kwa yeyote ambaye hatawatambua Maimam hawa: "Yeyote atakaekufa na asimjue Imam wa zama zake, atakufa kifo cha kipagani".

Taz: Sharhul Maqasid J. 2 Uk. 275

Al'mirqat J. 2 Uk. 509

Al'ghaadir J. 10 Uk. 260